Press Release

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimewataka wazazi, walezi, jamii hasa wanahabari kuchukua hatua na kulinda haki za wahanga wa ukatili wa jinsia na usalama wao katika mitandao ya jamii ili kuepusha udhalilishaji zaidi unaoweza kujitokeza.


TAMWA inachukua hatua hii baada ya kuendelea kusambaa kwa video fupi na maudhui, ya binti wa kidato cha tano wa shule ya Panda Hill mkoani Mbeya, aliyetoroka shule na kisha kudaiwa kukimbilia kwa mwanaume aitwaye Baba Jose.


Baada ya kusambaa kwa maudhui hayo, kumeendelea kusambaa video fupi na taarifa mbalimbali zikimuonyesha binti huyo akijieleza na kwenda mbali zaidi kuwa alifanyiwa ukatili wa kijinsia yaani kubakwa na mwalimu wake wa nidhamu, jambo lililovuta maoni mengi dhalili.


Hofu ya TAMWA inajikita zaidi katika utu, usalama, na hatma ya baadaye ya binti huyu ambaye mahojiano yake yanaendelea kusambaa huku wasambazaji na waandaji wa maudhui hayo wakiacha sura yake ionekane wazi wazi, jambo ambalo linavuta hisia na maneno dhalili yanayoweza kuweka usalama wake na afya yake ya akili hatarini.


TAMWA tunaamini kuwa binti huyu bado anayo nafasi ya kujenga hatma yake, hata kuendelea na masomo na baade kuwa mwanajamii mwenye mchango mkubwa kwa taifa.
Pia vyombo vya dola vilivyochukua maelezo yake ya awali vinauwezo wa kuhakikisha haki yake inapatikana vizuri zaidi kuliko mijadala inayozuka baada ya mahojiano yake na waandishi wasiofuata maadili na kusambaza mitandaoni.
Binti huyu bado ana haki ya kulindwa na wazazi, walezi, jamii, serikali na waandishi wa habari na ndio maana TAMWA tunapata wasiwasi anavyoendelea kuhojiwa na kusambazwa mitandaoni ambako kunazua hisia na mijadala dhalili, kutukanwa na kutuhumiwa.


Lakini pia, mpaka sasa inatushangaza kwani hatujaona wazazi au walezi wake wakisimama moja kwa moja kuzungumzia suala hilo na badala yake binti huyo ameachwa kujieleza peke yake kwa wanahabari ambao nao wameshindwa kulinda utu wa muathirika kwa mujibu wa maadili ya uandishi. Maadili ya uanahabari yanasisitiza kuficha sura ya waathrika wa ukatili hata ikiwezekana wazazi wa mtu/mtoto aliyefanyiwa udhalilishaji, ili kumlinda na kulinda utu wake na kumpunguzia maumivu ya ukatili aliopitia na katika hili binti huyu anastahili kulindwa.

Kwa mujibu wa kanuni zilizotengenezwa Baraza la Habari Tanzania (MCT,2020) ni kinyume cha maadili kuwabainisha watoto walionyanyaswa, kutumika vibaya au walioshtakiwa na kupatikana na hatia ya jinai. Kanuni hizo zinawataka waandishi wa habari kuchukua tahadhari katika kutumia picha na majina na waepuke kuchapisha taarifa kunapokuwa na uwezekano wa kuwaathiri wahusika.


Inaelezwa kuwa baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutoa amri ya kutafutwa kwa binti huyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera naye alitoa amri ya kusakwa. Alipopatikana taarifa zinaeleza kuwa, mwanamke aliyejitambulisha kama mama Abdul, ambaye naye alisema, binti huyo alipelekwa kwake na mwanaume mmoja aitwaye baba Jose, ambaye naye alisema: “Ni mke wake ...” Na baada ya hapo vyombo vya dola vilikusanya maelezo.

Katika hali hiyo TAMWA, kama wadau wa habari na watetezi haki za wanawake, wasichana na watoto, tunawataka wazazi, walezi , jamii na wanahabari kuwajibika na kulinda haki za wanawake na watoto, waliopitia ukatili wa kijinsia, ili kuepusha madhara ya kudumu na makubwa zaidi, ya kimwili na kisaikolojia kwa muathirika.


Imetolewa na


Dkt Rose Reuben

Mkurugenzi Mtendaji.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Machi 8, 2023, Dar Es Salaam. Leo dunia inaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Kwa mwaka huu, Siku hii inaadhimishwa ikipambwa na kauli mbiu isemayo, “Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia: Chachu Katika Kuleta Usawa wa Kijinsia”

Kauli mbiu hii inatukumbusha pengo lililopo katika teknolojia, kwa upande wa wanawake na watoto wa kike hasa nafasi ya teknolojia katika kuhakikisha usalama, amani, na usawa kwa kundi hilo.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Dar Es Salaam, Oktoba 11, 2022. Watanzania leo wanaungana na dunia nzima kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike. Siku hii inaadhimishwa  ifikapo Oktoba 11 kila mwaka kama wakati wa kukumbushana kuhusu nafasi ya mtoto wa kike katika nyanja mbalimbali, za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
 
 Hivyo basi kwa kuzingatia umuhimu wa siku hii, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kwa kushirikiana na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) tunaikumbusha jamii, wadau na serikali kuwa bado matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike yanaendelea kushika kasi nchini.
 
Kadhalika, kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu isemayo: Muda Wetu ni sasa, haki zetu, Mustakabali Wetu”. TAMWA na WFT tunalenga kuikumbusha jamii kuendelea kuibua na kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia, hasa rushwa ya ngono, ubakaji, ulawiti, vipigo na ndoa za mapema kwa watoto wa kike. 
 
TAMWA na WFT tumebaini kuwa licha ya  vyombo vya dola kuchukua hatua na kupinga vikali vitendo hivyo dhidi ya watoto wa kike lakini bado matukio ya rushwa ya ngono, ubakaji, ulawiti, mimba za mapema na udhalilishaji yanazidi kushamiri huku watuhumiwa wengi wakiwamo wazazi, walezi, walimu pamoja na watu wao wa karibu ambao ndio wamepewa jukumu la kulinda watoto hao.
 
Imeshuhudiwa kuwepo kwa matukio kadhaa ya ukatili wa kijinsia kwa  watoto  wa kike katika kipindi cha  Julai hadi  Septemba mwaka huu  jambo ambalo linatupa wasiwasi kuwa huenda elimu ya kulinda haki za mtoto wa kike bado haijawafikia wengi.
 
Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na lile la mwanafunzi wa darasa la saba, Shule ya msingi Shahende, Geita, Helena Mashaka (13) anayedaiwa kuchomwa  moto mikononi na mama yake hali iliyosababisha kushindwa kufanya mitihani yake ya darasa la saba. 
 
Kadhalika, mtoto Farida Makuya (16)  anadaiwa kuuwawa usiku wa Jumanne, Oktoba 4, 2022 nyumbani kwao Mtumba jijini Dodoma na watu wasiojulikana. 
 
Wakati huo huo, Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwabaka na kuwalawiti watoto zaidi ya 10 wa mafundisho ya kipaimara na kisha kuwapa fedha kiasi cha kati ya Sh 3,000 hadi 5, 000. 
 
Tukio jingine ni la mwanafunzi wa darasa la sita, (12), wa Shule ya Msingi Mbagala Kuu, Dar es Salaam,  anadaiwa kubakwa na Mwalimu wake, ambapo  Mwalimu huyo amekuwa akimpatia binti huyo ufunguo wa makazi yake binafsi ili endapo akimuhitaji aweze kufika kwake kwa urahisi.
 
Hata hivyo, tunaipongeza serikali kupitia vyombo vya sheria kwa kutumia muda mfupi kusimamia na kutoa hukumu dhidi ya mwalimu wa shule ya msingi ya Global, Dar es Salaam, aliyehukumiwa kifungo cha maisha kwa kubaka na kulawiti mwanafunzi wa miaka minane. 
 
Utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF) umebaini kuwa wasichana milioni 120, duniani wamewahi kulazimishwa kufanya ngono bila ridhaa yao.
 
Pamoja na ukatili huo kwa watoto wa kike, WFT na TAMWA  bado wanasisitiza jamii kuepuka rushwa ya ngono hasa kwa watoto wa kike. 
 
Mwaka 2020, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilichapisha ripoti ya utafiti na kuibua kuwepo kwa rushwa ya ngono katika Vyuo Vikuu viwili vya umma nchini, ambavyo ni Chuo kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)
 
Kadhalika, mwaka 2021, TAMWA kwa kushirikiana na (WFT) ilitekeleza mradi wa kuangazia rushwa ya ngono kwa wanahabari. TAMWA ilifanya utafiti na kubaini wanahabari wanakabiliwa kwa kiasi kikubwa na rushwa ya ngono na ukatili mwingine ndani ya vyombo vyao vya habari. 
 
TAMWA tumebaini kuwa wasichana wanahabari vyuoni  hukumbana na vitendo vya rushwa ya ngono na kusababisha wengi kuikimbia taaluma  hiyo wakihofia vitendo vya rushwa ya ngono ambayo hukumbana navyo kuanzia wakiwa vyuoni Mkurugenzi wa TAMWA, Dk Rose Reuben. 
 
TAMWA na WFT bado tunaendelea kuipongeza TAKUKURU kwa kufanya mabadiliko ya kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.  Hii ni dhamira chanya kwa serikali katika kushughulikia uovu huu katika nchi yetu. Kwa njia hii, inabakia kuwa sheria ya msingi katika kujenga msingi wa maadili ya taifa katika ngazi na taasisi zote. 
 
“Hata hivyo katika kifungu kidogo cha 2,cha sheria hii,  tumeona kuwa uchambuzi wa sheria unachanganya  neno ukahaba na ngono: Pale ambapo kuna makubaliano ya pande zote, ya kubadilishana ngono kwa ajili ya huduma, au pesa, (katika kesi hii hakuna unyang'anyi wa mamlaka). Hivyo tunaomba kuondolewa kwa kifungu kinacholeta utata kati ya rushwa ya ngono na ukahaba Rose Marandu, Mkurugenzi Mtendaji, WFT
 
Hivyo basi tunapoadhimisha siku hii ya mtoto wa kike, tunatamani dunia itambue thamani yao katika maendeleo, afya yao, elimu yao, uchumi wao na ushiriki wao katika siasa, jamii ikiutambua mchango wao, itasimamia katika ulinzi wao na hivyo kupunguza matukio haya ya rushwa ya ngono. 
Tunaomba serikali kupitia Takukuru, kuendelea kujikita katika mapambano haya wakishirikiana na wadau, ili jamii iwe na taarifa za kutosha kuhusu usalama wa watoto wa kike Rose Marandu,WFT
Hatutaacha, hatutanyamaza, hadi uwepo usalama wa watoto wa kike Tanzania!
 
 
Dkt. Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji
Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA)
 
 
Rose  Marandu
Mkurugenzi Mtendaji
Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT)
Mwisho

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Dar es Salaam, Juni 16, 2023. Watanzania leo wanaungana na dunia nzima kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, maadhimisho ya siku hii  yalianza mwaka 1991 baada ya kuteuliwa na Umoja wa Afrika katika kuenzi michango ya watoto walioshiriki maandamano Mjini Soweto, Afrika Kusini mwaka 1976 pamoja na kujengea jamii uelewa juu ya umuhimu wa elimu bora kwa watoto.

Kauli mbiu ya maadhimisho haya  kitaifa kwa mwaka huu ni “Zingatia Usalama wa Mtoto katika Ulimwengu wa Kidijitali” kauli mbiu hiyo inasisitiza kuwalinda watoto na kuwaongoza kwenye matumizi ya kidijitali ikiwemo simu za mkononi, kompyuta na runinga kwa kuwa vikitumika vibaya vinaweza sababisha  ukatili wa mitandaoni kwa watoto.

Siku ya Mtoto wa Afrika hutumika kuwakumbusha watoto wetu hatua ya kijasiri waliyoichukua wenzao huko Afrika Kusini katika kulinda haki zao. Watoto wanakumbushwa kwamba wanaweza kuleta mabadiliko hata wakiwa wadogo.

 Kwa hivyo, Siku Ya Mtoto wa Afrika inaadhimishwa kwa maslahi mapana ya watoto wa Afrika na inapaswa sisi watu wazima kujitolea kwa hali na mali katika nafasi zetu ili kushughulikia changamoto nyingi zinazokabili watoto katika bara zima na hasa hapa nyumbani Tanzania.

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) katika kuadhimisha siku hii, tunatoa rai kwa jamii kuweza kuongeza ulinzi kwa watoto kwa kuwakinga na vitendo vya ukatili  dhidi yao ikiwemo ukatili wa mitandaoni, mimba za utotoni, ndoa za utotoni, ulawiti, ubakaji, ukeketaji, unyanyapaa na ajira za watoto.

TAMWA kupitia tamko hili ambalo ni sehemu ya maadhimisho, kinamtaka kila mtu kwenye jamii kuwa chachu ya kutengeneza mazingira rafiki kwa watoto kuweza kutoa taarifa  endapo ataona viashiria vya ukatili vinavyofanywa na  mtu yoyote katika mazingira atakayo kuwepo mtoto ikiwemo ya mitandaoni.

Licha ya kuwepo kwa msukumo wa  mabadiliko ya teknolojia yanayopelekea watoto kuhamasika kutumia simu za mkononi, compyuta na runinga katika kupata taarifa, ni jukumu la kila mtu kuwafundisha watoto matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, pamoja na kuwepo kwa mazingira stahiki ili kuwalinda na ukatili ikiwemo udhalilishaji wa kimtandao,.

Katika mkataba wa haki za mtoto duniani uliopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa miaka 30 iliyopita umeonesha dhahiri unayosimamia zaidi  nguzo kuu nne ambazo ni haki ya kutobaguliwa, kuhakikisha mahitaji yake yanatimizwa, haki ya kuishi na kuendelezwa na haki ya kusikilizwa hivyo hatuna budi kuhakikisha tunatekeleza hilo.

Katika hali isiyo ya kawaida, nyumbani, shuleni, barabarani pamoja na nyumba za ibada zimekuwa ni sehemu zinazoripotiwa kwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto huku wanaokabidhiwa jukumu la kumlinda mtoto wakiwa ndio watuhumiwa wa matukio hayo wakiwemo  wazazi, walimu, walezi, ndugu pamoja na majirani.

Kwa mujibu wa Takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Tanzania kutoka Julai 2022 hadi Mei 2023, jumla ya mashauri 14,184 ya matukio ya Ukatili wa kijinsia kwa Watoto yalitolewa taarifa katika Vituo vya Polisi ikilinganishwa na matukio 12,642 yaliyotokea Mwaka 2021/22.

Aidha, Katika Hotuba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima alisema “kuanzia Januari 2022 hadi Machi 2023 jumla ya matukio ya Ukatili 15,901 yaliripotiwa Polisi. Kati ya matukio hayo Kesi 671 ndiyo zilifikishwa Mahakamani ambapo 368 zilizotolewa hukumu na kesi 303 zinaendelea”.

Aidha pengine kwa kuongezeka kwa matukio haya inadhihirisha  kuwa kuna muamko  kwenye jamii  katika kuripoti  masuala ya ukatili kwa watoto au pengine ni ongezeko la ukatili limezidi na si kwakuwa kuna mwamko wa jamii katika kuripoti matukio hayo.

 TAMWA tunatoa wito kwa jamii kuendelea kufichua vitendo hivyo katika vyombo vya usalama ili kutokomeza matukio hayo  dhidi ya watoto kwani mtoto wa mwenzio ni wako.

“Kutokomeza ukatili dhidi ya watoto ni jukumu la kila mtu na tusiruhusu mtoto wa kike kupoteza fursa ya elimu na kufurahia utoto wake kwa kumlazimisha kuingia katika ndoa akiwa na umri mdogo pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu, hivyo tunaihimiza Serikali kufanyia marekebisho sheria zote zinazokandamiza ustawi wa watoto ikiwemo sheria ya ndoa ya mwaka 1971”.Dkt Rose Reuben

“Ndoa za utotoni ni suala la afya pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu, kwani wasichana walioolewa kwa umri mdogo wana uwezekano mkubwa wa kuathiriwa  na fistula na vifo vya kina mama” Dkt Rose

Licha ya juhudi za Tanzania kukomesha ukatili dhidi ya  watoto, uelewa kuhusu kinga na mikakati kwa ujumla hautoshi. Ukatili dhidi ya watoto umefichua athari kubwa katika vipengele vya msingi vya afya ya kihisia, kitabia, na kimwili pamoja na maendeleo ya kijamii katika maisha yote na hasa katika mazingira ya elimu ambapo ujuzi wa mtoto unakuzwa.

TAMWA tunatoa wito kwa serikali yetu sikivu, jamii ya watanzania na wadau wote kushirikiana katika kushughulikia matukio ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ambayo yanaendelea kushamiri kwa kasi kubwa hapa nchini na duniani kote kama tunavyoshuhudia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Katika kumlinda mtoto wa afrika TAMWA tunaomba ushirikiano wa wadau wote wakiwemo wazazi, walezi, wanasheria, serikali kwa ujumla, wadau wa maendeleo kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha ulinzi na usalama wa watoto wetu ni wa uhakika na endelevu.

 “TAMWA tunampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri mwenye dhamana, ambao  wanaonesha wazi kuwa wanasimamia vyema haki za  watoto, tumewaona na kuwasikia wakipinga ukatili kwa watoto hatuna budi kusimama nao katika hili “ Dkt Rose Reuben

TAMWA katika kuadhimisha siku hii tunaendelea kufanya kampeni za kuelimisha na kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto kupitia vyombo vya habari na mitandao yetu ya kijamii. (Istagram @tamwa, Twitter @tamwa, pamoja na Facebook @tamwa Tanzania.

Kwa mawasiliano zaidi;

Tanzania Media Women Association (TAMWA)

P.O.BOX 8981, Dar es Salaam

Website: https://www.tamwa.org/

Find us @Facebook, twitter, instagram

Mobile: +255 22 2772681

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Novemba 29, 2022, Dar es Salaam. Miaka minne iliyopita, Chama cha  Wanahabari Tanzania(TAMWA) ilitekeleza mradi wake wa kuchapisha habari za uchunguzi juu ya unyanyasaji wa kingono mahala pa kazi na vyuo vikuu.
 
Mwaka mmoja uliopita, TAMWA ilitekeleza mradi mwingine uliofanana na huu, kwa kufanya utafiti kuangalia hali halisi ya rushwa ya ngono katika vyumba vya habari. 
Yote haya, yaliiwezesha TAMWA kubaini kuwa kuna tatizo  kubwa la rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono mahala pa kazi na katika elimu ya vyuo vikuu. Matokeo ya tafiti na uchapishaji wa habari kuhusu rushwa ya ngono, yalichagiza wadau na waathirika kuweka wazi hali halisi ya rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono katika mazingira ya kazi na elimu.  
 
Hivyo basi, leo wakati dunia inafanya maadhimisho ya Siku 16 kupinga ukatili wa jinsia,  yanayokwenda na kauli mbiu isemayo: Kila uhai una thamani, tokomeza mauaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
 
TAMWA  kwa kushirikiana na wanamtandao wa kupinga ukatili wa jinsia hapa nchini pamoja na  wadau wetu wa maendeleo  kwanza tunajisikia fahari kuibua mengi kuhusu athari ya rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono mahala pa kazi na katika taasisi za elimu na kwa kuendeleza mjadala huu katika jamii kupitia vyombo vya habari.
 
TAMWA kupitia miradi yake inayohimiza kuzuia ukatili katika jamii, tumeweza kufanya yafuatayo;
Kwanza, kuvunja ukimya uliotawala miongoni mwa wanahabari katika kusema kinagaubaga au kundika kuhusu madhila wanayopitia wanapodhalilishwa kingono.
 
TAMWA imebaini asilimia 48 tu ya wanahabari ndio wanaoweza kusema wazi kuhusu madhila ya rushwa ya ngono wanayopitia katika vyumba vya habari. Asilimia 52 inayobaki, hawawezi kusema wazi kuhusu changamoto hiyo.
Kadhalika TAMWA kwa kushirikiana na wadau wakiwamo Internews na WFT na Tasisi ya kuzuia Rushwa (TAKUKURU)wamebaini kuwa rushwa ya ngono katika vyuo vikuu ni janga kubwa linalochagiza kushuka kwa kiwango cha taaluma, kuzalisha wahitimu wasio na sifa na kuharibu talanta kwa wale wanaokataa rushwa hiyo. 
 
Tumebaini kuwa wanahabari wengi wanawake wameacha kazi kwa kuhofia udhalilishaji wa kijinsia katika tasnia hiyo, wapo wanafunzi waliohama vyuo na kuacha shule kwa kuombwa rushwa ya ngono.  
Kadhalika, imebainika kuwa wapo viongozi katika maeneo ya kazi, wanaotoa kazi kwa upendeleo kwa kuomba rushwa ya ngono badala ya kuangalia uwezo na vipaji. 
Juzi akifungua kongamano la wadau wa rushwa ya ngono kwa wanafunzi na wakufunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, jijini Dodoma, Naibu Waziri Utumishi, Deogratius Ndejembi, amesema rushwa ya ngono inasababisha kuzalishwa wasomi wasio na tija na kuwanyima haki wanafunzi.  
Kauli ya Ndejembi inachochea mjadala unaoonyesha  zaidi ukubwa wa tatizo hili na kutukumbusha watanzania  kuchukua hatua za ziada  kupambana na rushwa ya ngono mashuleni, vyuoni na katika sekta ya ajira na utumishi wa umma, tatizo ambalo linatishia kuharibu vipaji. 
“Hivyo basi, huu ni wakati kwa wadau wanaopinga ukatili wa  jinsia, watetezi wa haki za binadamu, wahanga wa ukatili na serikali   kukumbushana kuwa rushwa hii inavunja haki za binadamu, ni kosa la jinai kisheria, inaharibu utu, na inaua vipaji hapa nchini amesema Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dk Rose Reuben. 
 
TAMWA na WFT Tunaiomba serikali kama ambavyo tayari imeshaanza kulichukulia kwa uzito suala hili, iendelee kuwawajibisha wale wanaomba rushwa ya ngono kwa wanafunzi na kwa wafanyakazi.Kadhalika, , tunaomba wanafamilia, wanawake  na wanaume, vijana wa kike na wakiume na jamii kwa ujumla,  wadau wa kuzuia ukatili wa jinsia, wahanga wa rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono kushiriki katika mijadala inayoweza kuleta suluhisho la janga hili tupinge ukatili wa kijinsia na kuhamasisha uwazi zaidi. 
 
“Sote tunaweza kuwa watetezi na sauti zetu kwa pamoja zinaweza kuleta  mabadiliko tunayotafutaDr Rose Reuben.
 
Tunapoadhimisha Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, TAMWA tunatamani  kuwa asiwepo yeyote, popote pale, atakayefanyiwa  ukatili wa kijinsia hapa nchini. Lakini zaidi hasa tunasema; Rushwa ya ngono mahala pa kazi, vyuoni na mashuleni ni janga na inarudisha nyuma maendeleo ya jamii yetu.
Dr Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji
TAMWA.

Search